Nahitaji msaada
Ikiwa umeletwa Oman baada ya kupewa ahadi za uwongo, na hali zako za kazi ni tofauti sana na vile ulivyotarajia, huenda wewe ni mwathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu.
Je, kuna yoyote kati ya haya yanayokuhusu?
- Pasipoti yangu imechukuliwa.
- Mshahara wangu ni mdogo zaidi kuliko ule nilioahidiwa kwenye mkataba wangu.
- Ninalazimishwa kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi kuliko zilizoelezwa kwenye mkataba wangu bila malipo ya ziada.
- Siruhusiwi siku za kupumzika za kila wiki na silipwi fidia kwa kufanya kazi kwa siku zangu za kupumzika.
- Mwajiri wangu ananiambia nina deni lake la pesa kwa sababu ya kunidhamini pamoja na viza yangu.
- Mwajiri wangu anadai kuwa nina deni lake la malazi, huduma ya matibabu, au chakula.
- Nina deni la mdhamini wangu au wakala wa uajiri kwa kunileta nchini.
- Mwajiri wangu ametishia kunifukuza ikiwa nitawasilisha malalamiko kwa Polisi au Wizara ya Kazi kuhusu hali yangu ya kazi.
- Ninatendewa vibaya kingono au kuguswa vibaya na wanakaya ninakofanya kazi.
- Mwajiri wangu hunipiga.
- Nimetishiwa na vurugu.
- Ninalazimishwa kufanya mapenzi na wanaume.
- Nataka kuacha kufanya kazi kama kahaba na nirudi nyumbani lakini bosi wangu haniruhusu.
Ikiwa ndivyo, huenda wewe ni mwathiriwa wa usafirishaji haramu wa binadamu.
Na kumbuka wewe ni mwathiriwa, sio mhalifu.
Royal Oman Police iko tayari kukusikiliza. Wamefundishwa kuwasaidia watu kama wewe. Wanaweza kukulinda dhidi ya mwajiri. Wanaweza kukomesha mateso yako.
Nifanye nini?
Ikiwa unaruhusiwa kutoka nje peke yako, tembelea kituo cha karibu cha Royal Oman Police na uwaambie kilichokupata. Unaweza pia kumwomba rafiki yako awasiliane nao kwa niaba yako.
Simu zote hazina malipo. Maafisa huzungumza Kiarabu na Kiingereza.
Ikiwa huwezi kuzungumza Kiingereza au Kiarabu, mwombe mtu anayeweza kupiga simu kwa niaba yako.
Nini kitatokea basi?
Royal Oman Police watachunguza kesi yako. Wanaweza kukupeleka kwenye makazi maalumu kwa usalama na ustawi wako. Wafanyakazi wa msaada watahakikisha uko salama na watakupa makazi, huduma ya matibabu, na huduma nyingine unazohitaji kama mwathiriwa. Huduma zote hazina malipo.